Loading...

Madai: Aliyemuweka Mbongo rehani akamatwa!


DAR ES SALAAM: Mtanzania aitwaye Juma (jina lake la pili tunalihifadhi kwa sababu maalum) anayedaiwa kumuweka rehani ughaibuni Mbongo mwenzake Adam Akida Mwinyimkuu, mkazi wa Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam ambaye ametekwa na kushikiliwa na watu wanaoaminika kuwa ni ‘Wazungu wa Unga’ , amekamatwa na polisi jijini Dar.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Mihayo Msikhela
Uchunguzi wa kina uliofanywa na waandishi wetu wiki iliyopita umebaini kuwa, Juma alikamatwa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita Tegeta na anahojiwa kuhusiana na kutuhumiwa kumuweka dhamana kijana Adam kisha kumtelekeza ughaibuni huku ikidaiwa kuwa yeye alikuja na shehena ya unga.
Habari zinasema ili Adamu awe huru, Juma anatakiwa kupeleka fedha shilingi trilioni moja ambazo ni gharama ya unga aliopewa, huku akimfanya mwenzake huyo kuwa ‘bond’ ya mzigo huo haramu.
“Fedha anazodaiwa Juma ni nyingi ni shilingi trilioni moja. Ni kwamba mzigo wenyewe (unga) hakufanikiwa kuuza kwani alikamatwa na askari wakamnyang’anya na sasa sijui atafanya nini ili kumuokoa mwenzake aliye ughaibuni,” kilisema chanzo chetu.
Habari zaidi zinasema kuwa licha ya Juma kuwa korokoroni, baba wa Adamu mzee Akida Mwinyimkuu naye alishikiliwa kwa muda na polisi katikati ya wiki iliyopita lakini hakuwa na msaada wowote kwa vyombo vya dola.
“Mzee Akida alikamatwa na polisi lakini badala ya kusaidia akawa anapotosha ukweli. Yeye aliwaambia polisi kuwa mtoto wake Adam hakwenda Pakistani bali alikwenda Afrika Kusini na ndivyo anavyojua. Alipooneshwa video ya mwanaye akiwa chini ya ulinzi, alishangaa na hakuwa na la kusema,” kilisema chanzo chetu.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Mihayo Msikhela (pichani) alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kukamatwa kwa mzee Akida na Juma hakukiri wala kukataa.
“Unajua hili jambo bado lipo kwenye uchunguzi, hatuwezi kusema chochote hadi tumalize uchunguzi wetu lakini wote wanaotuhumiwa tunawasaka na tukiwakamata tutawahoji. Tukimaliza upelelezi wetu tutatoa taarifa kwa umma,” alisema kamanda huyo.

Mradi uliotumbua 6 NSSF ni huu!

DAR ES SALAAM: Wakati nafasi za wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) zilizoachwa wazi baada ya wahusika kusimamishwa zikiwa tayari zimejazwa, Uwazi limeuchimba kwa kina mradi uliowaponza vigogo hao waliosimamishwa hivi karibuni.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mwandishi wetu alifunga safari mpaka Dege, uliko mradi wa Ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni (Dege Eco Village) – (pichani) ambao unatajwa kuwa ndiyo uliosababisha kutumbuliwa kwa vigogo hao na kuzungumza na wakandarasi na wafanyakazi waliokuwa wakishiriki kwenye mradi huo.

WALIANZA HIVI
“Huu mradi kwa kweli ulikuwa na figisufigisu nyingi sana. Mimi binafsi nilikuwa nafanya kazi kama kibarua na kuna mambo mengi tu nilikuwa naona hayaendi sawa,” kilisema chanzo kimoja kilichoomba hifadhi ya jina lake.

Chanzo hicho kiliendelea kutiririka kwamba, kabla ya kuanza kwa mradi huo, eneo halikuwa na shughuli yoyote ya msingi lakini mradi ulipoanza, vigogo wengi serikalini, walianza kununua viwanja vikubwa kwenye maeneo ya kuzunguka mradi na kuporomosha majumba ya kifahari.
“Si unaona majumba ya watu binafsi yalivyoporomoshwa kwa wingi upande wa pili wa mradi? Hawa wote hakuna mkazi wa Dege hata mmoja, ni watu wa serikalini. Mradi wenyewe una magorofa kama 40 hivi,” kiliendelea kutiririka chanzo chetu.


MAFUNDI WALIUTABIRIA
Fundi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la James, yeye alisema walishajua kwamba mradi huo hauwezi kukamilika kutokana na mambo mbalimbali yaliyoashiria hivyo (hakuyasema).
 “Unajua kabla mradi haujasimamishwa, tulikuwa tunafanya kazi sehemu mbilimbili, yaani kwenye mradi na kwenye nyumba za baadhi ya vigogo wa serikalini. Kwa hiyo tulihisi kuna mambo hayaendi sawasawa sana.

“Mi naona hata serikali yenyewe ilichelewa kushtuka mapema. Lakini kwa vile wamesimamishwa, uchunguzi ufanyike kuona nani alikosa, naamini wapo waliosimamishwa hawahusiki lakini kuna wanaohusika, wapo kazini,” alisema fundi huyo.


Baada ya kusikia maelezo hayo, Uwazi lilifanya jitihada za kuwapata vigogo waliotumbuliwa. Hata hivyo, kazi ya kuwapata vigogo hao ana kwa ana haikuwa nyepesi.
Uwazi lilifanikiwa kupanga ‘appointment’ ya kukutana na Yacob Kidula, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi ambapo licha ya makubaliano ya kukutana, simu ya kigogo huyo haikuwa ikipatikana hewani na hata ilipopatikana, haikuwa ikipokelewa

Mwandishi wetu alifanya jitihada za kumtumia ujumbe wa maandishi kigogo huyo akimsisitiza kuhusu kukutana naye au kuzungumza chochote kuhusu kusimamishwa kwake lakini hakujibu mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni.
KUTOTAKA KUZUNGUMZA
Kuna taarifa kuwa, vigogo hao hawako tayari kuzungumza lolote kwa vile, suala lao linachunguzwa na vyombo husika ili kubaini ukweli wa madai yao na endapo wataonekana hawana hatia, watarudishwa kazini.


Hivi karibuni, bodi ya wadhamini ya NSSF inayoongozwa na Profesa Samuel Wangwe, iliagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa shirika hilo ili kupisha uchunguzi baada ya kubainika kuwepo kwa vitendo vya ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.


Wakurugenzi sita waliosimamishwa kazi na nafasi zao kwenye mabano ni Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha), Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala) na Sadi Shemilwa (Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga).
Wengine ni Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji) sambambana mameneja wengine watano na mhandisi mmoja.



Kabla ya kutumbuliwa vigogo hao, mradi huo ulisimamishwa na serikali Aprili, mwaka huu baada ya kubainika kuwepo kwa upotevu wa zaidi ya shilingi bilioni 179.
Mradi huo ulikuwa ukisimamiwa na Kampuni ya Hifadhi Builders LTD iliyokuwa chini ya NSSF kwa ushirikiano wa Azimio Housing Estate Limited, mkandarasi akiwa ni M/s Mutluhan Construction Industry Company Limited kutoka Uturuki.

Mgomo wa Madereva Daladala Mabomu ya Machozi Yarindima Mwanza

Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limelazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya madereva daladaa waliokuwa wamekusanyika na kugoma kusafirisha abiria mkoani humo.
Tukio hilo limetokea mapema leo jijini humo wakati madereva hao walipogoma kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwa madai kuwa wamekuwa wakitozwa kodi na faini za mara kwa mara bila kuzingatia sheria na kanuni za makosa ya barabarani.
Akizungumza na mwandishi wetu aliyeko jijini Mwanza, mmoja wa madereva hao waliokuwa wamekusanyika kwenye Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani cha Nyegezi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema wamechoshwa na vitendo vya askari wa usalama barabarani kuwatozwa kodi kila mara bila kuzingatia sheria wakati na wao (madereva) kipato chao kinategemea kazi hiyo.
Madereva hao wamezitaka mamlaka husika ziliangalie suala hilo kwa jicho la tatu ili waweze kufanya kazi zao kwa amani na uhuru bila manyanyaso.
Mbali na adha ya kupigwa mabomu ya machozi, mpaka saa 6 mchana, abiria walikuwa bado wapo vituoni wakihangaika kutafuta usafiri wa kuwapeleka kwenye shughuli zao huku wengine wakilazimika kutumia usafiri usio rasmi kwa kubanana kwenye gari aina ya Suzuki Carry maarufu kama ‘Virikuu’ na pikipiki za mizigo za magurudumu matatu.

Mtandao wa haki za binadamu walia na Jeshi la Polisi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwafikisha mahakamani wanachama wake wanne linaowashikilia kwa siku 12 sasa. 

Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo. 

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa wazi jambo lililo kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai. 

“Hadi sasa watetezi wanne wamenyimwa dhamana wakati wengine wenye nafasi za kisiasa wamepewa. Hii si sawa,” alisema Olengurumwa. 

Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa ni Samwel Nangiria, Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati walioachiwa ni mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros, Joshua Makko. 

Alieleza kuwa watetezi hao wamenyang’anywa vitendea kazi vyao pamoja na vifaa vya mawasiliano zikiwamo simu za mkononi na kompyuta mpakato. 

Wakili wa Kujitegemea wa kampuni ya Law Guards Advocates, Jebra Kambole alisema hiyo ni kinyume na sheria zinazosimamia haki za binadamu nchini. 

“Kumshikilia mtu muda mrefu bila dhamana pamoja na kunyimwa uwakilishi ni kinyume na Katiba ya nchi. Ni kinyume na Azimio la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998,” alisema Kambole baada ya kueleza kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa haki ya kuwatumia mawakili. 

Licha ya ombi hilo kwa Polisi, mwanachama wa mtandao huo, Rose Sarwatt alimuomba Jaji Mkuu kuingilia kati suala hilo ili kuhakikisha haki inatendekea. 

Aliziomba asasi za kimataifa kukemea na kuishauri Serikali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea huko Loliondo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jeshi lake linasimamia na kutekeleza sheria za nchi na halichagui wa kumkamata kama amefanya kosa la jinai.

 “Lazima ukamatwe labda uwe na kinga. Hata mimi, japo kazi yangu ni kukamata lakini nikifanya jinai nitakamwa tu,” alisema na kubainisha kuwa taratibu zinaendelea kuzingatiwa na zikimalizika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

Vikongwe wawili wauawa kwa tuhuma za uchawi

Vikongwe wawili mke na mumewe wa Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku nyumbani kwao.

Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75) ambao waliuawa na wananchi wakiwatuhumu kwa uchawi.

Msengi alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda, Jumamosi Mathias alisema kundi la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani kwa familia hiyo wakati wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.

Mathias alisema akiwa nyumbani kwake, alisikia kelele za watu wakisema; “Tumechoshwa na hawa wachawi. Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza kuhangaika ili kuona jinsi ya kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.

 Hata hivyo, alisema kabla ya kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya kinyama kwa vikongwe hao.

Alilaani kitendo kilichofanywa na watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee kwani tangu aishi nao kijijini hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi dhidi yao.

Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.

MWANADADA gumzo kwenye tansia ya Bongo Movie nchini Arejea CCM

MWANADADA gumzo kwenye tansia ya Bongo Movie nchini, Jacqueline Wolper hatimaye jana ametangaza rasmi kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wolper ambaye alikuwa kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mfuasi mkubwa wa aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa alitangaza uamuzi huo wakati wa hafla ya wasanii ya kumuaga Mwenyekiti Mstaafu Mhe. Jakaya Kikwete mjini Dodoma.
Baada ya kupewa nafasi kuongea, Wolper alikuwa na haya; “Nilipotea kwenda kule, nimeamua kurudi nyumbani”
Ikumbukwe kwamba Wolper alikuwa mstari wa mbele miongoni mwa wasanii wa kike nchini kumpigia debe bila kificho Edward Lowassa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana na alienda mbali zaidi kwa kumwita Edward Lowassa kama baba yake.

Dk Rehema Nchimbi-Iwe kwa usafiri wa baiskeli Viongozi wafikieni Wananchi Vijijini

MKUU wa mkoa wa Njombe Dk Rehema Nchimbi amewataka viongozi katika ngazi ya  halmashauri na wilaya mkoani humo kufanya kila liwezekanalo hata kwa kutumia usafiri wa baiskeli katika kuwafikia na kuwahudumia wananchi waishio vijijini badala ya kuendeleza mazoea ya kujifungia maofisini kwa kisingizio cha magari yao yamekosa mafuta.
Dk Nchimbi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo wakurugenzi watendaji wa halmashauri na wakuu wa wilaya mkoani humo ktk mkutano uliolenga kukumbushana vipaumbele vya mkoa huo na kuongeza kuwa kumekuwepo kwa tabia kwa baadhi ya viongozi kuacha kutekeleza majukumu yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa mafuta ktk vyombo vyao vya usafiri.
kwa upande wake Katibu Tawala mkoa wa Njombe Bw Jackson Saithabahu akisema ni vyema sasa kukawa na mikakati ya kuimarishwa kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kumaliza kero ya migogoro ya ardhi.

Mpango wa elimu bure umedaiwa kuanza kutumiwa vibaya

Mpango wa elimu bure umedaiwa kuanza kutumiwa vibaya baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi mkoani Simiyu kwa kuorodhesha idadi kubwa majina hewa ya wanafunzi  ili shule zao ziweze kupata fedha nyingi huku baadhi ya walimu wa madarasa wakitembea na madaftari ya mahudhurio kwa kuhofia kuongezewa majina hewa.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa wa simiyu  Antony Mtaka amewaagiza wakurugenzi na wakuu wa wilaya kufanya uhakiki wa wanafunzi hewa na watakaobanika kufanya hivyo wawajibishwe.
Agizo hilo amelitoa katika kikao kazi  cha wadau wa  elimu mkoani simiyu kilichokuwa kikijadili  tathimini fupi ya elimu na kutoa dira ya elimu na mikakati madhubuti ya kutatua changamoto zilizopo ambapo ufaulu umepanda kutoka asilimia 40 na kufikia asilimia 60 kitaifa.
Mtaka amesema kuwa wapo baadhi ya wakuu wa shule wasio waaminifu wamekuwa wakiongeza  majina wanafunzi hewa  ili fedha hizo zinazokuja za elimu bure waweze kujinufaisha hivyo lazima uhakiki ufanyike na watakaobainika kuwajibishwa.
Akizungumza mara baada ya majadiliano hayo mkuu wa wilaya ya meatu Dk joseph chilongani ameahidi kutekeleza agizo la kudhibiti utoro mashuleni kwani hakuna kisingizio cha mwanafunzi kukosa mahitaji ya lazima huku akikisitiza kuhakiki wanafunzi hewa.

Alichokiandika Zitto Kuhusu Hotuba ya Mrema na Cheyo Jana

Kufuatia hotuba walizotoa Augustino Mrema na John Momose Cheyo jana katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma haya ndiyo aliyoyaandika Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook;
Unashangaa ya Mrema ( TLP ) na Cheyo (UDP)? Kama ni msomaji wa Siasa za Dunia wala hutasumbuka maana NI mambo yamefanyika sana. Hao ndio systemic opposition.
Jambo la muhimu ni kujua kuwa Rais wa sasa sio yule aliyemtangulia na hivyo CCM ya kuanzia Leo haitakuwa CCM iliyoishia Jana. Rais anayeweza kutamka hadharani kuwa ‘angewapoteza’ watu, tena wanachama wa Chama chake, kwa kuonyesha kutokukubaliana na Maamuzi ya chama ndani ya vikao vya Chama, ni mtu hatari na hivyo mbinu za kushindana naye lazima 

Huu ndio wakati wa kujenga Mfumo madhubuti wa Vyama vingi kuliko wakati mwengine wowote katika historia ya Nchi yetu. Nasaha zangu kwa Viongozi wote wa upinzani ni ‘ tujisomee kwanza ‘! Tujue mbinu na medani. Pia Sisi tuwe ‘ more democratic ‘ kuliko CCM kwa kuruhusu maoni tofauti kwenye Vyama vyetu badala ya kuwa na tabia zile zile za CCM.
Mrema na Cheyo wamekuwa wenyeviti wa Vyama vyao tangu Mwinyi ni Mwenyekiti wa CCM na bado hawaoni haya wala soni kusifia CCM na mfumo wao wa kubadilishana Uongozi. Cheyo alikuwapo Mwinyi alipomkabidhi Mkapa, Mkapa alipomkabidhi Kikwete na Kikwete alipomkabidhi Magufuli! Kote huko alitoa hotuba. Wachambuzi wa Siasa wangechambua hotuba za Cheyo miaka yote hiyo na kumwuliza anajisikiaje!

Uenyekiti wa Magufuli CCM ni faida kwa mfumo wa Vyama vingi kwani Upinzani wa kweli utaimarika. Upinzani wa Hoja na Masuala utaimarika zaidi kuliko wakati mwengine wowote.
Huu ndio wakati wa kusambaza Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha.

Gwajima Afunguka atoa ya moyoni

Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Uzima na Ufufuo ameshiriki misa pamoja na
waumini wakeDar es Salaam. Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Uzima na Ufufuo ameshiriki misa pamoja
na waumini wake.

Askofu huyo aliyeondoka nchini Juni 15 kwenda Japan, alikuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi
baada ya kusambaa kwa sauti iliyorekodiwa ikihusishwa naye, ikitoa tuhuma za kuwapo mipangoya kumzuia Rais John Magufuli asipewe uenyekiti wa CCM kutokana na kazi anayoifanya ya

kushughulikia mafisadi.Kwenye misa hiyo ya kwanza tangu arejee nchini, Gwajima hakuizungumzia Serikali wala taasisizake na badala yake alijikita kutoa mafundisho ya kuwajenga waumini wake kuweza kukabiliana

na changamoto za duniani zinazokwamisha maendeleo yao kiroho na kimwili.
"Mwenyezi Mungu habadili mipango yake. Ni binadamu pekee ndiye anaweza kukupa leo na
akakunyang’anya kesho,” amesema wakati akihubiri.

Dk Ali Mohamed Shein, amefuta uteuzi wa Naibu Kamishna wa ZRB

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amefutauteuzi wa Naibu Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Hafidh Ussi Haji hukuakimteua Khadija Shamte Mzee, kuchukua nafasi hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein,amefuta uteuzi wa Naibu Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Hafidh Ussi Haji huku
akimteua Khadija Shamte Mzee, kuchukua nafasi hiyo.

Pia, taarifa ya Ikulu inaonyesha Dk Shein, amemteua Amour Hamil Bakari kuwa Kamishna waBodi ya Mapato Zanzibar kuchukua nafasi ya Abdi Khamis Faki ambaye anastaafu kwa mujibu wa
sheria.Vilevile, Dk Shein amemteua Umi Aley kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika 

Magazeti ya Serikali; Said Bakar Jecha na Sebtuu Mohammed Nassor wameteuliwa kuwaMakamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wakati Ali Saleh Mwinyikai ameteuliwa

kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji Zanzibar.
Wengine walioteuliwa ni Maryam Hamdan kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa na Sensa yaFilamu na Utamaduni, wakati Maryam Abdulla Yussuf ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la

Mitihani Zanzibar na Profesa Ali Seif Mshimba, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi yaWakurugenzi ya Shirika la Viwango Zanzibar. Uteuzi huo unaanza Julai 25.

Serikali yapiga: Marufuku viberiti Na Mishumaa Mabwenini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na heater za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitembelea Shule ya Sekondari Lindi baada ya shule hiyo kuteketea kwa moto hivi karibuni.
“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Waziri Mkuu amesema kwa namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema yakavunjwa na kujengwa upya ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga madarasa mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, mama Salma Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na wanafunzi waliosoma shule hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali nchini kufunga vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia pindi ajali za moto zinapotokea.
Older Posts
© Copyright TanzaBongo | Designed By Code Nirvana
Back To Top